Wednesday, May 1, 2013

VIGOGO CCM WAMJIA JUU MKUU WA MKOA ARUSHA,WADAI AMEMWONGEZEA UMAARUFU LEMA, CHADEMA



VIGOGO wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiwemo wabunge, wamemjia juu Mkuu wa Mkoa (RC) wa Arusha, Magessa Mulongo kwa jinsi alivyoshughulikia kesi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA).

Wabunge hao waliliambia gazeti hili mjini Dodoma kuwa kesi ya uchochezi iliyofunguliwa na serikali dhidi ya Lema kwa shinikizo la mkuu huyo, itaiathiri kwa kiasi kikubwa CCM.

Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alisema kuwa amefuatilia kwa makini chanzo cha kesi ya Lema na hatimaye kukamatwa na polisi mithili ya gaidi, na kubaini kuwa hulka za utendaji kazi wa baadhi ya viongozi wa serikali zinawapa sifa na umaarufu zaidi CHADEMA.

Mimi sitaki kuingilia kesi, lakini ukiangalia kuanzia ile inayoitwa video ya vurugu za Chuo cha Uhasibu Arusha na jinsi Mkuu wa Mkoa alivyofika eneo la tukio na kuondoka, utabaini udhaifu mkubwa wa kiongozi huyo ambao leo unamfanya Lema aonekane shujaa.

Leo tunaingia kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani pale Arusha, tunaweza tukashinda, lakini tutafanya kazi ya ziada kwa sababu tu ya udhaifu wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha,” alisema Lugola.
Mbunge mwingine ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema alichokifanya Mulongo ni sehemu ya tatizo kubwa la viongozi wa serikali kujihusisha na ukereketwa wa kisiasa.

Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa kuna kiongozi, tena hakumtaja jina, kwamba anapendwa kubebwa, alisema mwacheni abebwe. Alisema vile kuwazuia polisi kukabiliana na watu wanaopenda kumbeba kiongozi huyo.

Mkuu wa Mkoa Arusha na wengine wanaokabiliana na wapinzani kwa nguvu kubwa bila sababu, hii inawaongezea umaarufu,” alisema mbunge huyo kutoka moja ya majimbo ya kanda ya kati.

SOURCE CHADEMA BLOG

0 comments:

Post a Comment