Katika gazeti la
Mtanzania toleo na. 7269 la Jumatano Machi 27, 2013 kuna habari yenye kichwa
chenye maneno ‘ SIRI YA KUUAWA ZITTO YAFICHUKA’ na
vichwa vidogo ‘yadaiwa ilipangwa anyweshwe sumu hotelini’ dk. Slaa atajwa
kumtuma Saanane kummaliza’. Habari hii imeniletea usumbufu mkubwa kwani ndugu,
jamaa, marafiki na wapiga kura wangu, wamejazwa na wasiwasi mkubwa sana kwamba
ninaweza kuuwawa. Napenda kusema yafuatayo:
Moja, sijawahi katika maisha yangu yote
kukutana na mtu anayeitwa Ben Saanane na hivyo hicho kikao ambacho inasemekana
nilikuwa naye na akajaribu kunipa sumu hakijawahi kutokea. Imetajwa Hoteli ya
Lunch Time ambayo sio tu sijawahi kufika, pia hata siijui ipo wapi. Haijawahi
kutokea mimi kufanya kikao cha pamoja na Ben Saanane, Juliana Shonza na Mtela
Mwampamba. Hivyo habari iliyoandikwa ni ya kufikirika na hivyo naomba mwandishi
ahakikishe kuwa vyanzo vyake vya habari vimempa habari sahihi.
Pili, Siamini kamwe kuwa Katibu Mkuu wa
chama changu anaweza kupanga kuniua maana hana sababu ya kufanya hivyo. Napenda
kurudia kusema kwamba mimi ninaamini kuwa kila nafsi itaonja mauti. Kila mtu
atakufa. Kama nitakufa kwa kuuwawa na mtu mwingine ndio itakuwa nimeandikiwa
hivyo na Mungu.
Ndio maana hata siku moja silalamiki kuhusu
vitisho vya kuuwawa nk. Kama kuna mtu anafikiria kuwa kumuua Zitto ndio furaha
ya maisha yake atakuwa anajidanganya tu maana Zitto anaweza kufa kimwili lakini
mawazo, fikra na maono ya Zitto yataishi tu. Siogopi kufa maana maisha
niliyoyachagua ndio haya ambayo yamejaa vitisho. Muhimu kwangu ni kufanya kazi
zangu kwa bidii, uhodari na uaminifu. Siku zote nitasimamia ukweli bila kujali
uchungu wa ukweli huo.
Tatu, nawashauri watu ambao wamehama
CHADEMA na kuhamia vyama vingine watumie muda wao kujenga vyama vyao badala ya
kila siku kuzungumzia masuala ya chama ambacho wao sio wanachama tena. Kama mtu
kaamua kuhama CHADEMA anapoteza haki ya kujadili masuala ya CHADEMA maana kama
angekuwa anapenda kuyajadili asingehama. Naonya mtu yeyote ambaye anatumia jina
langu ili kufanikisha malengo yake ya kisiasa. CHADEMA sio pango la watesaji
wala wauaji. Kama kuna mwanachama wa chama kingine cha siasa anayedhani kuna
mtu ndani ya CHADEMA anapanga mipango ovu aende kwenye vyombo vya sheria
kumshtaki. Matendo ya mtu mmoja yasifanyiwe propaganda kama ni malengo ya
taasisi.
Nne, Nawashauri viongozi wa CHADEMA na
hasa wanachama tutumie muda wetu kujenga mshikamano ndani ya chama. Fitna,
majungu, uongo, uzandiki nk kamwe havijengi chama. Chama chetu lazima kiwe
mfano bora wa kuheshimu demokrasia na haki za binaadamu. Wananchi hawawezi
kutoa dola kwa chama chenye mifarakano. Tusiruhusu kugawanywa kwa matakwa ya
watu wachache. Tusimamie misingi ya kuanzishwa chama chetu.







0 comments:
Post a Comment