Wednesday, October 15, 2014

SINA REKODI YA KUFUNGWA NA YANGA-PHIRI

Kocha Mkuu wa Simba, Mzambia, Patrick Phiri, amesema rekodi yake nzuri katika mechi dhidi ya watani wa jadi ndiyo 'itakayowamaliza' wapinzani wao Yanga katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambayo itafanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Simba iko jijini Johannesburg, Afrika Kusini kujiandaa na mchezo huo ambao huvuta hisia za mashabiki wa soka ndani na nje ya nchi.

Akizungumza kwa njia ya simu Phiri ambaye katika misimu miwili tofauti aliyoinoa Simba kabla ya huu amefungwa mara moja tu na Yanga, alisema kambi ya Simba huko Afrika Kusini haiangalii mechi moja dhidi ya watani hao wa jadi, ila ni maalumu kurejesha morali kwa wachezaji msimu huu na haifikirii timu hiyo peke yake.

Phiri alisema amefurahishwa na maamuzi yaliyofanywa na viongozi wa klabu hiyo kuipeleka timu Afrika Kusini kujiandaa na kujipima na klabu za huko hali inayowapa wachezaji nafasi ya kupata uzoefu na mbinu mpya za kuwakabili washindani wake.

"Ni nafasi pekee na adimu kwa timu za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kupeleka timu zao Afrika Kusini kujiandaa, wengi huogopa gharama lakini matokeo mazuri yanatokana na kuwekeza," alisema Phiri.

Kocha huyo alisema kuwa anaamini matokeo ya kambi hiyo yatapatikana na si kwa kuangalia mechi hiyo ya Jumamosi peke yake.

"Nimekuta ligi ina changamoto tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma, nimejifunza na nitaendelea kujifunza ili kukiboresha kikosi, tunamatumaini ya kufanya vizuri mechi zinazofuata," aliongeza Phiri.

Kuhusiana na suala na nani atadaka katika mechi ya Jumamosi kutokana na makipa wake, Ivo Mapunda (alikuwa majeruhi) na Hussein Shariff 'Casillas' naye kuumia, litajulikana Ijumaa jioni.

Phiri jana alizuia timu hiyo kucheza mechi ya kirafiki na badala yake leo ndiyo itashuka kuikabili Jomo Cosmos.

0 comments:

Post a Comment