Wednesday, April 2, 2014

NIPO TAYARI KUONDOKA YANGA-KASEJA

Kipa Juma Kaseja amesema yuko tayari kuondoka Yanga kufuatia kuelemewa na tuhuma kwamba anaifungisha timu hiyo aliyojiunga nayo akitokea kwa mahasimu
wao wa jadi, Simba.

Kaseja amekuwa katika wakati mgumu kutoka kwa mashabiki wa Yanga ambao hawaamini kama magoli anayofungwa ni ya kimchezo na kwamba hata makipa wakubwa duniani hufungwa. 

Kaseja alisema anasikitishwa na tuhuma za kuihujumu Yanga na kueleza kwamba soka ni mchezo wa makosa hivyo hastahili kupewa lawama hizo.

"Naumia na maneno hayo, sijafanya makusudi kufungwa, ni goli ambalo nilijitahidi kuruka hadi mwisho wa uwezo wangu, kwani mimi siwezi kufungwa? Mbona kuna watu walikosa penalti (Misri) lakini hakuna aliyelaumiwa?" alisema Kaseja.

Alisema kwamba yeye ni kipa mzoefu na ana uwezo kwa kucheza lakini makosa yanayotokea uwanjani ni ya kimchezo kama wanavyofanya wachezaji wengine wa ndani na wa timu za Ulaya.

Aliongeza kuwa tatizo kubwa linalowakabili wanachama, mashabiki na viongozi wa klabu za Simba na Yanga ni kutokubali kufungwa na timu pinzani.

"Mimi sihusiki na mambo hayo, nimeanza kucheza mpira siku nyingi na wengine wanaosema hawakuwapo kwenye soka, kama sitakiwi niambie mapema, kama (alitaja jina la timu) ndiyo wananituma, mbona wenyewe hawajiwezi," alihoji kipa huyo.

0 comments:

Post a Comment