nchini, Emmanuel Okwi, hajajihakikishia namba kikosini humo na kwamba uamuzi wa kumpanga au kutompanga katika mechi za ligi na za kimataifa za timu hiyo utatokana na uwezo atakaouonyesha mazoezini.
Okwi aliyesajiliwa Yanga kwa dola 150,000 (Sh. milioni 240) katika uhamisho uliojaa utata kutoka katika klabu ya SC Villa ya Uganda aliyokuwa akiichezea kwa kibali maalum cha FIFA akitokea El Merreikh ya Sudan, anatarajiwa kuanza kuitumikia klabu hiyo ya Jangwani katika mechi ya ligi Jumamosi dhidi ya Ruvu Shooting baada ya Shirikisho la Soka Nchini (TFF) kuelezwa na FIFA kwamba mshambuliaji huyo anaweza kuitumikia klabu yake mpya licha ya kuwapo kwa kesi mbalimbali zinazomhusisha.
Akizungumza na gazeti hili jana, Pluijm alisema kuwa kamwe hawezi kumpanga mchezaji kwa kuangalia ukubwa wa jina au umaarufu wake na hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa Okwi ambaye sasa anatarajiwa kuanza kuitumikia Yanga.
Pluijm alisema kwamba mchezaji atakayefanya vizuri mazoezini ndiye atakayejihakikisha namba kwenye kikosi chake na hizo ndiyo sera zake katika klabu zote alizowahi kufundisha.
"Mazoezi yanaendelea na kila siku nafurahi kuona wachezaji wanazidi kuimarika, wote wanafahamu tuna majukumu magumu yanayotukabili mbele, tunatakiwa kujiimarisha kila idara ili tuweze kufanya vizuri," alisema kocha huyo wa zamani wa klabu ya Berekum Chelsea ya Ghana.
Naye kocha msaidizi, Boniface Mkwasa, aliliambia gazeti hili kwamba wameamua kwenda kuwaona 'live' wapinzani wao Al Ahly ili kupanga mikakati ya kuwamaliza katika mechi yao ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayofanyika Machi Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa.
Mkwasa ambaye alitarajiwa kuondoka nchini jana usiku kuelekea Cairo alisema kuwa wakiwa huko pia watapata nafasi ya kujua mbinu nyingine za wapinzani wao za nje ya uwanja kwa kukutana na wadau wa soka wanaoifahamu timu hiyo katika msimu huu.
"Tumeona ni vyema kwenda Cairo kuwaona na kuacha kutegemea mikanda ya video, naamini tunaweza kufanya vizuri na kusonga mbele, sasa hivi hakuna kuhofia jina la klabu, kila timu inaweza kuibuka na ushindi," aliongeza Mkwasa.
Alisema pia baada ya kuwaona wapinzani wao ndiyo watajua kama wanahitaji kuongeza muda wa mazoezi au waendelee na programu ya mara moja kwa siku ambayo wanaifanya sasa.
Mkwasa anatarajiwa kuishuhudia Al Ahly kesho Alhamisi ikiikaribisha CS Safaxien ya Tunisia katika mechi ya fainali ya Super Cup itakayochezwa jijini Cairo.
Yanga imesonga mbele katika mashindano hayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kuisambaratisha Komorozine ya Comoro kwa jumla ya mabao 12-2 katika hatua ya awali.
Wakati huo huo, TFF imewalalamikia wana familia watano wa mpira wa miguu kwa Kamati ya Maadili kuhusiana na udanganyifu katika mtihani wa utimamu wa mwili wa waamuzi na usajili wa mchezaji Emmanuel Okwi.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa Riziki Majala na Army Sentimea ambao ni wakufunzi wa waamuzi, na Oden Mbaga na Samwel Mpenzu ambao ni waamuzi wanadaiwa kughushi nyaraka kuhalalisha mtihani huo kinyume cha taratibu.
Naye Sabri Mtulla analalamikiwa na TFF kwa madai ya kuidanganya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kuwa hakukuwa na pingamizi lolote juu ya usajili wa mchezaji Emmanuel Okwi huku akijua wazi kuwa jambo hilo si kweli.
Kwa mujibu wa kanuni, malalamiko hayo yamefikishwa kwenye Kamati ya Maadili ambayo itachunguza ili kujiridhisha kama yana msingi au la. Ikibaini kuna kesi ndipo walalamikiwa watafika mbele ya kamati hiyo.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment