Mwanadada anayetamba na miondoko yake ya 'kiuno bila mfupa', Rehema Chalamila 'Ray C', ameishauri serikali kutunga sheria kali dhidi ya wauza dawa za
kulevya ili kuinusuru jamii ya Watanzania kutumbukia katika ubugiaji wa 'unga' aina nyingine za dawa hizo.
Akizungumza katika kipindi cha 'Mkasi' kilichorushwa na EATV usiku wa kuamkia jana, Ray C aliyekuwa akitesa katika anga la muziki wa kizazi kipya, alishauri Tanzania itunge sheria kali dhidi ya wauza unga ikiwamo ya kuwanyonga watu wanaopatikana na hatia ya kujihusisha na biashara hiyo haramu.
"Nafikiri kuwe na sheria kali zaidi kudhibiti biashara hiyo, China wanawanyonga kwa nini isiwe Tanzania?" Alihoji Ray C, ambaye alipotea katika fani ya muziki takriban miaka mitatu kutokana na athari za matumizi ya unga.
"Namshukuru sana baba yangu Rais Kikwete (Jakaya) kwa kunisaidia, kwa kweli yule baba ana roho nzuri. Siyo mimi tu, amesaidia watu wengi kuondokana na balaa hili la dawa za kulevya. Kuna wafanyakazi wa benki wametumbukia kweye dimbwi hili," alisema Ray C.
LANGA, NGWEA
Aidha, mkali huyo wa muziki wa kizazi kipya aliyekuwa katika upinzani mkali na mwenzake, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’, alisema anawakumbuka sana washikaji zake wanamuziki marehemu Langa na Ngwea huku akiweka wazi kwamba walikuwa wenzake katika utumiaji unga.
"Sikuhudhuria mazishi ya Langa na Ngwea, lakini 'nawamiss' (nawakumbuka) sana washikaji zangu hao. Kwa kweli wangelikuwa hai ningelikuwa nawapitia 'twenzetu' Mwananyamala Hospitali kunywa 'Methadone' (dawa wanaomeza watu walioamua kuachana na ubugiaji wa unga)," alisema.
"Ukitaka kukosana nami, ongea mabaya kuhusu sisi (walioachana na matumizi ya unga). Kwa kweli nitakuchukia sana kwa sababu hili ni janga la taifa, linaweza kumkuta ndugu yako, mwanao au yeyote. Tumeamua kuweka wazi ili tusaidiwe. Mimi kwa sasa ni balozi wa mambo haya, dawa (Methadone) zipo hospitali ya Mwananyamala na Muhimbili na zinaendelea kusambazwa nchi nzima kuokoa Watanzania," alifafanua zaidi Ray C.
AREKODI NYIMBO 12 MPYA
Katika hatua nyingine, Ray C, ambaye amekuwa na umbo kubwa kwa sasa, alisema unene haumsumbui na 'mauno' yako pale pale. Alisema amejipanga vizuri kuhakikisha anarejesha heshima yake katika fani ya muziki kwa kuachia 'vitu' vikali.
"Sijawahi kuharibu nikiingia studio. Mpaka sasa nimesharekodi nyimbo 12 mpya, mashabiki wangu na Watanzania wasubiri uhondo tu," alitamba Ray C kisha akaweka wazi kwamba kwa sasa hayuko tayari kuwa na uhusiano na 'vitoto' na atakuwa tayari tu kuolewa na 'mtu mzima mwenye busara na anayejitambua'.
CHANZO: NIPASHE







0 comments:
Post a Comment