Mwenyekiti
wa klabu ya soka ya Simba, Ismail Aden Rage amesema hana mpango wa
kutetea kiti chake katika Uchaguzi Mkuu ujao wa klabu hiyo kutokana
na kuchoshwa na hali na vurugu klabuni hapo.Rage alisema kama hali ya vurugu ndani ya Simba itaendelea kuna uwezekano mkubwa wa kuuitisha mapema uchaguzi huo kabla ya kuanza kwa duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara badala ya kufanyika Mei mwakani kama inavyotakiwa.
Akihojiwa na katika kipindi cha michezo cha kituo cha redio cha jijini Dar es Salaam, Rage alisema anafikiri kuitisha uchaguzi huo mwezi ujao ili Simba ipate viongozi wapya kamili kusaidia kumaliza vurugu zinazoendelea ambazo zinaelekezwa kwake.
Rage alisema katika uchaguzi huo ujao hatagombea nafasi yoyote kwa sababu muda alioiongoza klabu hiyo umemtosha kwa namna alivyoandamwa kutokana na misimamo yake ya kudhibiti mapato na miaya yote iliyowanufaisha 'walaji'.
"Sifikiriii kugombea tena nafasi yoyote Simba kwani vurugu zimenichosha, kuna watu wanakerwa na msimamo wangu wa kuziba mianya iliyowanufaisha baadhi ya watu, ili klabu inufaike na mapato yake," alisema Rage mmoja wa wenyeviti machachari waliowahi kuiongoza Simba kwa miaka ya karibuni.
Rage alisema kwamba hali ya amani ikishindwa kutulizwa ndani ya klabu hiyo anatarajiwa kuitisha mkutano mkuu wa uchaguzi wa viongozi wote haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kupata uongozi mpya ili kuinusuru klabu hiyo.
"Nadhani uchaguzi huo utaifanya Simba iwe na mwenyekiti mpya, makamu mpya na kamati mpya ya utendaji itakayoingia kwenye duru la pili kwa salama ili kuisaidia timu ifanye vyema katika Ligi Kuu," alisema.







0 comments:
Post a Comment