Monday, December 16, 2013

MILLIONI 355 ZIMEMLETA OKWI YANGA

Mshambuliaji mpya wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga, Mganda Emmanuel Okwi, amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea klabu
Yanga kwa thamani ya shilingi milioni 355.2 za Tanzania.

Okwi ambaye amewahi kuichezea Simba kabla ya klabu hiyo kumuuza Etoile du Sahel ya Tunisia kwa Dola 3,000 za Kimarekani sawa na Sh. milioni 480 za Tanzania ambazo hata hivyo hadi leo Wekundu wa Msimbazi hao wanadai hawajalipwa, Yanga imeipata saini yake kwa kiasi cha Dola za Marekani 150,000 sawa na Sh. milioni 240 za Tanzania.

Mbali na dau hilo, pia atakuwa akilipwa mshahara wa Dola za Marekani 3,000 kila mwezi ambazo ni sawa na Sh. milioni 4.8 za Tanzania, huku akipatiwa malazi na usafiri binafsi wa kutembelea.

Hivyo, Sh. milioni 4.8 atakazozilipwa kwa mwezi zitamfanya katika mkataba wake wa miaka miwili kuvuna jumla ya Sh. milioni 115.2 ambazo ukijumlisha na dau lake la usajili la Sh. milioni 240, zinamfanya hadi atakapomaliza mkataba wake wa miaka miwili, kuitumbua Yanga jumla ya Sh. milioni 355.2.

0 comments:

Post a Comment