ZIARA ya mikoa 10 ya kimuziki yenye lengo la
kuupa nguvu muziki wa Kitanzania na utamaduni wake kwa ujumla, ilianza juzi
katika viwanja vya Jamhuri mkoani Dodoma na kujumuisha wanamuziki saba
wanaong'ara katika tasnia ya muziki Tanzania huku wakongwe na chipukizi
wakitoana jasho.
Ziara hiyo iliyodhaminiwa na kampuni ya bia
ya TBL kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro, ilijumuisha wanamuziki
mchanganyiko kama Judith Wambura, Linex Sunday, Roma Mkatoliki, Ommy Dimpoz,
Kala Jeremiah, Profesa Jay na mkali wa muziki wa R&B nchini Ben Pol.
Wanamuziki waliotia fora katika tamasha hilo
ambalo wiki ijayo linatarajia kuelekea katika mkoa wa Tanga ni Ben Pol ambaye
alikuwa wa pili kupanda jukwaani. Mashabiki walionekana dhahiri kumuelewa na
kuitikia kila wimbo aliokuwa akiimba na kusababisha wakati mwingine yeye kukaa
kimya na kuachia mashabiki hao waimbe mwanzo hadi mwisho wa wimbo.
Ben Pol alipanda na wimbo 'Maneno Maneno' na
kusababisha shangwe kubwa uwanjani, na baada ya hapo, aliimba nyimbo zake
maarufu kama 'Pete', 'Jikubali', 'Samboira', 'Nikikupata' na 'Maumivu'.
Lady Jaydee alikuwa ni mwanamuziki mwingine
aliyeshangiliwa sana, baada ya kupanda jukwaani akiwa bila bendi, jukwaa ambalo
aliacha kupanda kwa takriban miaka saba sasa, mara baada ya kuanzisha bendi
yake ya Machozi.
Jaydee alipanda jukwaani na wimbo aliomshirikisha
marehemu Albert Mangweha, ambapo baada ya kumaliza alisema ni heshima yake kwa
kijana huyo ambaye ameacha alama katika muziki wa kizazi kipya nchini. Baada ya
hapo aliendelea na vibao kama 'Wangu', ambapo alikuwa akiimba na kurap
mwenyewe, hali iliyosababisha uwanja mzima wa Jamhuri kushangilia muda wote
aliokuwa akiimba.
Ulipofikia wakati wa kuimba wimbo wa 'Joto
Hasira', akasindikizwa na Profesa Jay ambaye alizidi kupagawisha maelfu ya wakazi
wa Dodoma waliokuwa wamefurika uwanjani hapo kuangalia uzinduzi wa ziara hiyo
ya muziki ya Kili ambayo mwaka huu haijumuishi washindi wa tuzo kama ilivyo
kawaida, bali wasanii wanaong'ara katika medani ya muziki wa kizazi kipya.
Akiongea baada ya onesho hilo, Meneja wa Bia
ya Kilimanjaro, ambaye alionekana kufurahia onyesho alifafanua kwamba kampuni
yake, kupitia bia ya Kilimanjaro imedhamiria kuupeleka muziki wa Tanzania
katika hadhi yake na ndio maana mwaka huu, imebeba mandhari ya kikwetukwetu,
ili kuipa sanaa ya Kitanzania nafasi ya kutambulika.
Ziara hiyo inatarajia kuendelea wiki ijayo
katika mkoa wa Tanga kabla ya kuelekea Moshi wiki inayofuata.
sOURCE NIPASHE







0 comments:
Post a Comment