Mshindi wa Tuzo ya Msanii Bora, Diamond Platnumz ni
miongoni mwa wasanii nyota sita wa muziki wa kizazi kipya watakaotumbuiza bure
mbele ya maelfu ya mashabiki katika tamasha la wazi liitwalo 'Tigo Mini
Kabaang' litakalofanyika Jumapili kwenye viwanja vya CCM Kirumba jijini Mwanza.
Akizungumzia tamasha hilo jana jijini Dar es Salaam,
Meneja wa Chapa ya Tigo, William Mpinga, alisema lengo la tamasha hilo ni
kuwapa burudani mashabiki wa muziki jijini Mwanza na pia kujenga mahusiano ya
karibu na wananchi kupitia sanaa ya muziki.
Mpinga aliwataja wasanii wengine nyota watakaokuwapo
katika tamasha hilo kuwa ni Madee wa Tip Top Connection, Ney Wamitego, Roma
Mkatoliki, Rich Mavoko, Recho, Kazi Kwanza na Fid Q.
Akizungumzia tamasha hilo, Diamond alisema kuwa yeye na
wenzake wanafurahia tamasha hilo la wazi la Tigo kwani litawapa nafasi ya
kuwakutanisha na mashabiki wao wa jiji la Mwanza.
“Nina furaha ya kipekee kufanya tamasha kubwa la wazi
jijini Mwanza, naamini mashabiki wangu
waliokuwa wakitamani kuniona lakini
wakishindwa kutokana na viingilio vya kwenye kumbi, sasa watapata nafasi
kupitia tamasha hili la Tigo,” alisema Diamond.
Source: Nipashe







0 comments:
Post a Comment