Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kwa gharama yoyote
kipo tayari kumtetea Mkurugenzi wake wa Ulinzi na Usalama, Wilfred
Lwakatare dhidi ya kesi ya ugaidi inayomkabili.
Lwakatare
na mwenzake, Joseph Rwezaura, wanakabiliwa na kesi ya ugaidi katika
Mahakama ya Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka manne ya kula njama na
kufanya mipango ya kumteka, kisha kumdhuru kwa sumu, Mhariri Mtendaji
wa gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky.
Majalada
hayo namba 37 na namba 6 yote ya mwaka 2013, yalishawasilishwa
Mahakama Kuu, kwa awamu mbili. Jalada la kwanza, namba 37
liliwasilishwa Mahakama Kuu, Jumatatu na jalada la pili namba 6
liliwasilishwa Jumanne wiki hii iliyopita.
Mkurugenzi
wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema, Tundu Lissu alisema kuna
wanaohoji nguvu ya kisheria wanayoitumia kuweka jopo la mawakili
watano kumtetea Lwakatare, akisisitiza kuwa wapo tayari kuhakikisha
sheria inatumika ipasavyo kubainisha ukweli wa tuhuma hizo.
Lissu
aliyasema hayo jana alipokuwa akieleza msimamo wa baadhi ya mambo
yaliyojadiliwa na Kamati Kuu kwenye kikao chake kilichofanyika Dar es
Salaam.
Pia,
alisema wanamwamini Jaji Lawrence Kaduri aliyepangwa kusikiliza
maombi ya kupinga utaratibu wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP). “Jaji
Kaduri aliyepangwa kusikiliza kesi hii aliwahi kuwa Mkurugenzi wa
Mashtaka (DPP) miaka kadhaa iliyopita, hivyo tunaamini kwa uzoefu
wake alionao kwenye masuala ya sheria ataamua kwa kuzingatia sheria,”
alisema.






0 comments:
Post a Comment