Tuesday, October 8, 2013

HIVI NDIVYO TUNDU LISU ALIVYOTETEWA BAADA YA JK KUMCHANA ETI NI MNAFIKI

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amekumbusha kwamba hotuba yoyote inayowasilishwa bungeni na
Waziri Kivuli ni ya kambi hiyo na siyo hoja ya mbunge anayeisoma.

Mbowe aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua mkutano wa siku nne wa wataalam mbalimbali wa Chadema kutoka kanda za kichama.

Alisema haikuwa sahihi kwa Rais Kikwete kumshambulia Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, wakati wa hotuba yake ya mwisho wa mwezi kwa sababu alisoma kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani. Lissu pia ni Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria wa kambi hiyo.

“Lissu alitimiza wajibu wake wa kikanuni ndani ya Bunge kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani, kwa hiyo kitendo cha Rais kumshambulia na kulitangazia Taifa uhasama na Lissu hakumtendea haki na kwa mtu muungwana anapaswa kumwomba radhi Lissu,” alisema.

Alisisitiza kwamba taarifa ya Lissu kuhusu kutoshirikishwa Zanzibar kwenye mchakato wa maoni kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na ile ya uteuzi wa wajumbe, haina uongo wowote.

Mbowe alisema hata baada ya wabunge wa upinzani kuomba mwongozo na kunyimwa fursa hiyo hadi wakaamua kutoka nje, wabunge wa CCM waliobaki ndani hawakujadili muswada badala yake walirusha vijembe na kejeli kwa kambi ya upinzani.

0 comments:

Post a Comment