Mshambuliaji
wa nyota wa zamani wa timu ya soka ya Simba na Taifa, Joseph Kaniki
‘Golota’ na bondia Mkwanda Matumla wanashikiliwa huku Addis
Ababa, Ethiopia wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya.
Kaniki na Matumla walikamatwa Agosti 31, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Bole, Addis Ababa wakati wakijiandaa kupanda ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia tayari kwa safari ya kuelekea Paris, Ufaransa.
Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Samuel Shelukindo alithibitisha jana kwamba wanamichezo hao wanashikiliwa nchini humo na Polisi wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai.Wanamichezo hao wamepandishwa kizimbani katika Mahakamu Kuu ya Ethiopia iliyoko kwenye eneo la Arada, Addis Ababa kujibu tuhuma za kubeba kilo saba za dawa hizo haramu. Mkwanda anadaiwa kubeba kilo nne wakati Kaniki akidaiwa kubeba kilo tatu. Kama watapatikana na hatia, wanaweza kufungwa kifungo cha miaka tisa hadi 15.
Alisema uwezekano wa kesi ya Kaniki na Matumla kurudishwa Tanzania haupo kwa kuwa nchi hizi mbili hazina utaratibu wa kubadilishana wafungwa.
“Wameshikiliwa hapa Ethiopia kwa zaidi ya siku 10 sasa, sisi tulipigiwa simu na polisi wa hapa Alhamisi iliyopita kujulishwa kwamba kuna Watanzania wawili wameshikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya, tulipokwenda tukamkuta ni Kaniki na Matumla,” alisema Shelukindo.







0 comments:
Post a Comment