Thursday, July 4, 2013

TUNAJUTA KUMUUZA OKWI-SIMBA



Klabu  ya soka ya Simba  imesema kuwa inajutia kitendo chake cha kumuuza mchezaji Bora katikati ya msimu uliopita aliyekuwa mshambuliaji hatari kikosini, Emmanuel Okwi na kuwaathiri kiufundi kiasi cha kumaliza  Ligi wakiwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa mwisho wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kitendo kilichopelekea kupoteza ubingwa waliokuwa wakiushikilia.

Simba ilitolewa pia katika hatua ya awali ya michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kupokea kipigo cha jumla ya mabao 5-0 kutoka kwa Recreativo de Libolo ya Angola.

Okwi aliuzwa kwa  pesa nyingi sana  dola za Marekani 300,000 (Sh. milioni 480) kwa klabu ya Etoile du Sahel inayoshiriki Ligi Kuu ya Tunisia, fedha ambazo zimebaki kuwa hadithi kwani hadi sasa Simba haijalipwa na Waarabu hao.

Aden Rage, alisema kuwa kuondoka kwa Okwi kulichangia kuiyumbisha klabu yao katika mzunguko wa pili wa ligi kuu msimu uliopita kwani nyota huyo anayetegemewa pia na timu ya taifa ya Uganda (The Cranes) alikuwa ni miongoni mwa wachezaji muhimu kikosini mwao.

Rage alisema jambo jingine ambalo Simba halitarudia ni kuuza mchezaji kwa 'mali kauli' kwani wamejifunza kutokana na namna wanavyozungushwa fedha  zitokanazo na mauzo ya Okwi; na ambazo kuzikosa kuliifanya klabu yao ishindwe kusajili nyota waliowatarajia msimu huu.

1 comments:

  1. Huu ni unafiki na upuuzi wa kiwango cha juu,hivi kweli ilihitaji busara kubwa kiasi gani kuliona kuwa lilikuwa kosa kubwa kuliko jinai kumuuza Okwi,huku tena timu ikiwa mashindanoni klabu Bingwa Afrika,achilia mbali Ligi kuu.Hapa akili iliyotumia lazima ni ya matope.

    Jambo la kusikitisha eti Jamaa yetu aliwahi kucheza mpira,tena akachezea Simba,kumbe kucheza soka na kuongoza kilabu ni vitu tofauti kama usiku na mchana.Okwi kwa misimu miwili mfululizo kila Kagame Cup ikifanyika alikuwa sijui wapi kwenye majaribio,hivi kweli hawakuwahi kuona kama ni makosa makubwa walikuwa wakifanya kumuuza bila replacement ya uhakika ambayo ilitakiwa ifanywe kwanza kabla ya kuuza mchezaji muhimu kama Okwi.

    Mimi ninapendekeza Kujuta kuambatane na kuachia ngazi ili maisha yaweze kuendelea kwa upande mwingine.Kumbuka Jamaa aliwahi kuwa Katibu mkuu mwanzoni mwa miaka ya80,enzi za Diagonal na Canivosamba.Miaka zaidi ya thelathini baadae Mshikaji hana jipya na ameonyesha kwa Vitendo kuwa hawezi.Ni vema aondoke kwa heshima kwa sababu haihitajiki nguvu ya Umma kama ya Tahrir Square.

    ReplyDelete