MTOTO mchanga ameliwa
na mbwa na kubakishwa mguu, baada ya mtu
asiyejulikana kukitelekeza kichakani katika eneo la Magole, mtaa wa Kivule, Manispaa
ya Ilala, jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo la
kusikitisha limebainika baada ya mbwa huyo kukibeba kiungo hicho kutoka
kilipokuwa na kukifikisha nyumbani anakofugwa majira ya sita mchana juzi.
Mwenye mbwa huyo
aliyejitambulisha kwa jina la Maria John, aliiambia NIPASHE kuwa, kabla ya kupelekwa
mguu huo, jana yake mbwa huyo alikwenda na utumbo ambao hata hivyo hakuna
aliyekuwa na hofu nao, kwani walidhani ni
wa kuku.
“Niliona ni kitu cha
kawaida tu, mbwa hutembelea maeneo mbalimbali labda ameokota mzoga wa kuku, lakini
leo (juzi) nilipoona mguu nilistaajabu na kufahamu kuwa ni kiungo cha binadamu
nilitoa taarifa kwa majirani na kupata msaada,” alisema.
Alisema lengo la
kutoa taarifa kwa majirani zake ni ili waweze kujadiliana na kutamfuta aliyefanya kitendo hicho cha
kikatili kisha baadaye kutoa taarifa kwa mjumbe wa mtaa huo.
Mmoja wa majirani
waliokusanyika kushuhudia tukio hilo ambaye hakupenda jina lake liandikwe
gazetini, alisema hajawahi kushuhudia tukio kama hilo.
“Ni tukio la
kushangaza na kusikitisha sana kwa mtu kukatisha maisha ya kiumbe kisicho na
hatia,kwani huwezi kujua mungu alimpangia nini duniani, hivyo kwa kweli kama
mama najisikia uchungu sana,” alisema.
Mjumbe wa Serikali ya
Mtaa wa eneo hilo, Grace Martin, alisema alipigiwa simu na mdogo wake kuwa,
mbwa ameokota kiungo cha mtoto na
kutakiwa kurudi mtaani hapo haraka.
“Nilipofika
nilihakikisha kuwa kweli ni mguu wa mtoto, niliamua kumpigia simu Mwenyekiti wa
Mtaa kwa ajili ya msaada,”alisema.
Mwenyekiti wa
Serikali ya Mtaa wa Kivule,Joseph Gassaya alisema yeye alipojulishwa alitoa
taarifa kwa Jeshi la Polisi kituo cha Stakishari Ukonga nao baada ya muda mfupi
walifika eneo la tukio.
Alisema askari
walitoa amri ya kukizika kiungo hicho katika eneo hilo, huku Jeshi la Polisi
likiendelea na upelelezi wa kumsaka mama aliyefanya ukatili huo ili afikishwe
kwenye vyombo vya sheria.
SOURCE NIPASHE
0 comments:
Post a Comment