Aliyekuwa
Kocha Mkuu wa Simba, Abdallah 'King' Kibadeni ameingia mkataba wa
nusu msimu kuifundisha timu ya soka ya
Ashanti United katika mzunguko
wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom.Hivi karibuni Kibadeni na aliyekuwa msaidizi wake, Jamhuri Kihwelu 'Julio' walitimuliwa kuifundisha Simba na nafasi yake kuchukuliwa na kocha kutoka nchini Croatia, Zdravok Logarusic ambaye naye jana amejifunga kuinoa timu hiyo kwa mkataba wa nusu msimu (miezi sita).
Afisa Habari wa Ashanti United, Marijan Rajabu, alisema Kibadeni amesaini mkataba jana na uongozi wa klabu hiyo, na leo anatarajia kukutana na wachezaji katika Ukumbi wa Hoteli ya Lamada kwa ajili ya kufahamiana na kupanga siku ya kuanza mazoezi.
Aliongeza kuwa, uongozi wa timu hiyo umeamua kumwajiri kocha huyo ili kuongeza nguvu na kuinasua timu hiyo isishuke daraja.
Alisema kikao hicho cha dharura kimepangwa na kocha huyo pamoja na benchi la ufundi la Ashanti United inayoshika nafasi tatu kutoka mkiani ikiwa na pointi 10 baada ya kucheza mechi 13 za mzunguko wa kwanza.
Alifafanua zaidi kuwa, mara baada ya ya kikao cha leo timu hiyo inatarajia kuanza mazoezi katika Uwanja wa Msimbazi Rovers jijini Dar esSalaam kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom.
0 comments:
Post a Comment