Tuesday, May 21, 2013

SERIKALI KUANZISHA BENKI YA VIJANA YA TAIFA


Serikali iko katika hatua za awali za uanzishwaji wa benki ya Vijana ya Taifa ambapo hivi sasa unafanyika uchambuzi wa michanganuo (Proposal) iliyowasilishwa katika hatua za kumpa mshauri mwelekezi.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Profesa. Elisante Ole Gabriel alisema tayari taasisi tisa za kitaalamu zimeshajitokeza na kuwasilisha michanganuo yake.

Profesa. Ole Gabriel alisema msingi wa kuanzishwa kwa benki ya Vijana unatokana na muendelezo wa kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ulioanzishwa katika mwaka wa fedha wa 1993/94.

Alisema Mfuko huo umeshakopesha zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kwa SACCOS za vijana kati ya mwaka 2009 na 2012, fedha ambazo kwa kiasi kikubwa zimewasaidia vijana kuinua hali zao za kiuchumi.

Alisema nia ya Serikali kutaka kuanzisha benki ya vijana si kujipatia faida kwa kufanya biashara bali lengo kubwa ni kutaka kubadili hali ya maisha ya vijana (economic status) ili kuwafanya vijana waweze kukabiliana na hali ngumu ya maisha.

Alisema benki hiyo itakuwa tofauti na benki nyingine kwa kuwa yenyewe itakuwa ikitoa mikopo maalum kwa ajili ya vijana pekee. Aliongeza kuwa vijana wanapofikisha umri wa miaka 35 hubaki kama wateja wa kawaida.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, benki ya vijana itaongeza utambuzi kwa vijana kwenye mfumo wa uchumi kwa kuwa itakuwa ikitoa mafunzo ya moyo na mbinu za ujasiriamali ili vijana waweze kulipa mikopo watakayokopeshwa.

Wakati huo huo Idara ya vijana imeanzisha kanzidata (database) itakayowawezesha kufahamu vijana wako wapi, wanafanya nini na wanashauri nini kifanyike ili kuboresha maendeleo ya vijana.

Katika hili, Idara ilisambaza madodoso maeneo mbalimbali nchini.
Alisema vijana 4,699 tayari wameshajibu madodoso hayo kuonyesha wako wapi na mikoa ya Singida na Tanga ndiyo inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya vijana walioitikia zoezi hilo.

Aliipongeza mikoa hiyo na kuitaka mikoa mingine kuiga mfano huo.
Alisema mpaka sasa vikundi 176 vimeshawasilisha taarifa zake na kati ya hivyo vikundi 98 vimesajiliwa na vikundi 76 havijasajiliwa.

Source Habari Maelezo

0 comments:

Post a Comment