Mshambualiaji nyota
wa zamani wa timu za Simba na Taifa Stars, Mussa Hassani Mgosi
anayeichezea kwa sasa JKT Ruvu, amesema yupo tayari kutua katika timu
yoyote ikiwamo Simba na Yanga, mradi aridhishwe na masilahi
atakayoafikiana na klabu husika.
Aidha, mshambuliaji
huyo alisema amefurahi mno kuisaidia JKT Ruvu kunusurika kushuka
daraja, lakini amekiri kwamba klabu hiyo haikuwa na msimu mzuri mwaka
huu kwa namna ilivyoyumba na kupoteza makali iliyokuwa nayo kwa
misimu kadhaa ya nyuma.
Mgosi aliyewahi
kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Motema Pembe ya DR Congo,
alisema kwa vile mkataba wake wa mwaka mmoja na JKT Ruvu unamalizika
mwisho wa msimu huu, atakuwa huru kutua katika klabu yoyote
itakayomhitaji.
Mgosi alisema
hatajali ni timu gani itakayomhitaji kwa msimu ujao, mradi
wakubaliane kimasilahi kwa kuwa yeye ni mwanasoka na ajira yake
inategemea mchezo huo.
Aliongeza kuwa hata
kama JKT Ruvu itamhitaji aendelee kubaki hatakuwa na pingamizi kwa
vile ni moja ya timu anazozipenda na alishawahi kuichezea zamani
kabla ya kurejea safari hii na kuitumikia tena.
"Niko tayari
kutua kokote kwa msimu ujao, sitabagua timu hata kama ni Mbeya City,
Ashanti, Simba au Yanga, muhimu ni masilahi tu," alisema.
Mfungaji bora huyo
wa zamani wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na michuano maalum
iliyofanyika China mwaka jana, alikiri ligi ya msimu huu ilikuwa
ngumu na isiyotabirika japo anasikitika vibali kumkwamisha kuishiriki
tangu mzunguko wa kwanza baada ya kurejea kutoka Congo.
Source:Nipashe
0 comments:
Post a Comment